KONA YA SHERIA

ULEVI SIO UTETEZI JUU YA KOSA LA JINAI
KWA kawaida ulevi sio utetezi dhidi ya kosa lolote lile la jinai (F. 14(1). Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Isipokuwa ulevi unaweza kuwa utetezi iwapo kutokana na ulevi huo wakati wa kutenda kosa linalodaiwa mshitakiwa hakuelewa lile alilokuwa akilifanya (F. 14(2). Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Ni muhimu mshitakiwa athibitishe kuwa hali hiyo ya ulevi ilisababishwa na mtu mwingine kwa sababu ya uzembe wake au makusudi bila ya ridhaa yake. Au mshitakiwa athibitishe kwamba kutokana na ulevi huo alirukwa akili kwa muda au kipindi chochote kile.


Utetezi wa ulevi hautumiki sana katika idadi kubwa ya mashitaka ya jinai isipokuwa mauaji. Na hakika, kwa masikitiko makubwa, washitakiwa wengi wamefanikiwa kuutumia utetezi huu kwenye mashitaka ya mauaji ya kukusudia. Badala yake wameonekana na hatia ya kuua bila ya kukusudia (Angalia R.v. Retiff (1941) 8 E.A.C.A 71. Pia Attoney General of Northern Island v. Gallaghar (1961) 3 ALL ER. 299, Athumani Mrisho v. R. (1956) 23 E.A.C.A. 532, Nyakite Oyigi v. R. (1959) E.A. 322, Canisio Wahwa v. R. (1950-51) 17 E.A.C.A. na R.v. Justo Odima (1941) 7 E.A. 29).


Idadi kubwa ya mauaji, hasa vijijini, husababishwa na ulevi. Tatizo ni vigumu kuelewa kwa usahihi iwapo wakati wa mauaji yenyewe au kosa lolote lile mshitakiwa alikuwa amelewa kweli kiasi cha kutoelewa analolitenda au la. Aghalabu upande wa mashitaka hushindwa kuthibitisha bila shaka ya maana kwamba mshitakiwa hakuwa mlevi wakati wa mauaji au kosa lolote lile linalohusika. Na kama kawaida, mahakama hutumia upungufu huo wa ushahidi kwa manufaa ya mshitakiwa.


Ulevi sio lazima usababishwe na pombe. Madawa kadhaa huweza kusababisha ulevi. Hata hivyo pombe hubakia kuwa njia kuu ya ulevi. Utetezi huu unaingiliana kidogo na ule wa kichaa maana walevi wengine hupotewa na akili.


Umri mdogo


Mtoto chini ya umri wa miaka saba hawajibiki kwa kosa lolote lile la jinai (F.15, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Dhana ni kuwa katika umri huo mtoto hajui kabisa kuainisha jema na baya. Dhana hii haikanushiki hata pale ambapo inaelekea mtoto ametenda kosa fulani kwa makusudi.


Aidha, mtoto chini ya miaka kumi na mbili hawajibiki kwa kosa lolote la jinai. Lakini dhana hii inaweza kukanushwa kwa ushahidi kwamba wakati wa kutenda kosa linalohusika mtoto huyo alikuwa na uwezo wa kujua kwamba kutenda kosa hilo ni vibaya. Watoto wengine hukomaa akili mapema kuliko wengine kwa hiyo sio busara kuwaona watoto wote chini ya miaka kumi na mbili kuwa na uwezo wa kujua au kutokujua ubaya wa yale wanayoyatenda. Hilo ni suala la ushahidi.


Mwanaume chini ya miaka kumi na mbili hawajibiki kabisa kwa makosa ya zinaa (F. 15, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Dhana isiyokanushika kisheria ni kwamba katika umri huo mwanaume hana uwezo wa kumjamii mwanamke. Lakini katika maendeleo ya sasa dhana hii ya kisheria inaonekana pungufu kwani watoto hukua haraka zaidi kuliko zamani. Hakika wengi wao hufanya mapenzi kwa siri wakiwa na umri wa chini ya miaka kumi na mbili. Dhahiri kipengele hiki cha sheria kimetupwa nyuma na wakati.


Shuruti


Mtu hawajibiki kwa kosa la jinai ambalo amelitenda kwa kushurutishwa (F. 17, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Ni lazima mshitakiwa athibitishe kuwa wakati wote wa kutenda kosa hilo alikuwa ameshurutishwa kwa vitisho vya kumwua mara moja au kumjeruhi vibaya. Vitisho vya baadaye sio udhuru wa kutenda kosa kwa sababu ni dhahiri mhusika anaweza kukwepa madhara hayo ya baadaye.


Kujitetea


Katika kujitetea mtu hawajibiki kwa kosa lolote iwapo wakati huo anatumia nguvu za kutosha kujihami yaani kujiepusha na madhara yanayomkabili (F. 7, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Daima nguvu zinazotumika kujitetea zilingane na kiasi cha shambulio lenyewe. Rungu kwa rungu, shoka kwa shoka. Sio ngumi kwa bastola, matusi kwa panga. Nguvu au aina ya kujitetea isiwe zaidi ya inavyostahii katika mazingira ya shauri lenyewe. Hata hivyo kila shauri litaamuliwa kufuatana na shauri lenyewe. Hata hivyo kila shauri litaamuliwa kufuatana na mazingira yake. Inawezekana mtu akawa sahihi katika kutumia bastola kumwua mwizi ambaye ameingia ndani ya nyumba yake na kutishia usalama wake hata kama mwizi huyo hakuwa na silaha ya hatari. Mtu hangojei kushambuliwa ndipo ajitetee. Anaweza akafanya hivyo kabla ya kushambuliwa, kwa namna au nguvu zaidi inavyostahili kutokana na imani kuwa asipofanya hivyo anaweza kudhurika vibaya sana.


Kwa jinsi hiyo hiyo mtu anaruhusiwa kumtetea mtu mwingine.


Iwapo kifo kinatokea kutokana na matumizi ya nguvu isiyolingana na shambulio lenyewe mshitakiwa anaweza kupatikana na hatia ya kuua bila ya kudhamiria.


Utetezi wa mali


Licha ya kuruhusiwa kujitetea mwenyewe au mwenzake mtu anayo haki sawa na hiyo katika kutetea mali yake (K.h.j.).


Kuhutubia Mahakama


Mwisho wa utetezi wake mshitakiwa anayo haki ya kuyahutubia mahakama. Katika kufanya hivyo huonyesha sababu ambazo ama kisheria, au kutokana na uchache wa ushahidi, anastahiki kutopatikana na hatia.


Tatizo lililo ni kuwa wengi hawaitumii nafasi hiyo. Wale wanaoitumia hawafanyi hivyo kikamilifu. Hawawezi kuyahutubia mahakama vizuri kwa maana ya kuonyesha athari za upande wa mashitaka ambazo zastahili kuwafanya wasipatikane na hatia. Inashauriwa kuwa mawakili wa pande zote, kama wapo, kuitumia nafasi hiyo vizuri, sio kuongezea chumvi na kuyapotosha mahakama. Na wajibu wa mahakama kuwa macho na mbinu za aina hiyo hasa pale upande mmoja unapokuwa hauwakilishwi na wakili.

0 comments:

Post a Comment